Bingwa wa mbio za Olimpiki kwa Watu Wenye Ulemavu Duniani Oscar Pistorius anatarajiwa kufikishwa mahakamani mwezi wa Machi mwaka ujao akikabiliwa na mashtaka ya kumuua mpenzi wake katika Siku ya Wapendanao.
Mwanariadha huyo raia huyo wa Afrika ya Kusini mwenye umri wa miaka 26 ambaye hana miguu yote miwili, anakabiliwa na hukumu ya kifungo cha maisha iwapo atapatikana na hatia.
Pistorius amepandishwa tena kizimbani ikiwa ni miezi sita tangu kumpiga risasi na kumuuwa mpenzi wake Steenkamp katika choo cha nyumba yake ilioko Pretoria alfajiri ya tarehe 14 mwezi wa Februari.
Mwanariadha huyo hivi sasa yuko nje kwa dhamana na alikiri kumuuwa mpenzi wake huyo lakini amekanusha kwamba alifanya hivyo kwa kukusudia, akisema kwamba alimpiga risai kupitia mlango wa choo uliokuwa umefungwa kwa kumdhania kuwa ni mwizi.