Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua maabara ya mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ( Tehama) ya chuo Kikuu huria cha Tanzania katika kituo cha Uratibu cha Chuo hicho kilichopo Zanzibar Beit El- Ras Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif akiwapongeza wanafunzi wa Kituo cha uratibu cha chuo kikuu Huria Tanzania kilichopo Beit El Ras kwa uamuzi wao wa kujipatia mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza mara baada ya kuzindua maabara ya mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ya chuo Kikuu huria cha Tanzania katika kituo cha Uratibu cha Chuo hicho kilichopo Beit El- Ras Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mara baada ya uzinduzi wa maabara ya mafunzo ya (Tehama) ya chuo Kikuu huria cha Tanzania katika kituo cha Uratibu cha Chuo hicho kilichopo Zanzibar. (Picha na Hassan Issa wa –OMPR– ZNZ).
Vijana Nchini wametakiwa kuchangamkia fursa za elimu zinazotolewa na vyuo mbali mbali nchini ili kupanda daraja la kitaaluma, pamoja na kuwa na uwezo wa uchanganuzi wa mambo tofauti yatakayosaidia Kitaifa katika kupanga na kutekeleza mipango ya kimaendeleo kwa ustadi.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizindua maabara ya mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ya Chuo Kikuu huria cha Tanzania katika kituo cha Uratibu cha Chuo hicho cha Zanzibar Beit El- Ras Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif amesema jamii imeshuhudia mabadiliko makubwa ya haraka ya sayansi na teknolojia yaliyosababisha baadhi ya wafanyakazi katika taasisi tofauti za umma na hata zile za kibinafsi kuachwa nyuma kwa kutofahamu matumizi ya taaluma hiyo.
Ameuomba uongozi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania uendelee kusogeza fursa hiyo karibu zaidi na wananchi kama ilivyo dhamira ya Chuo hicho katika miaka kumi ijayo, ambapo Vituo vya Uratibu kama cha Zanzibar vitabahatika kuwa Chuo kwa kushirikiana na Mikoa husika.
Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua kuwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimewakomboa wananchi wengi nchini kwa kuwafikishia elimu ya Cheti, Stashahada, Shahada ya Kwanza pamoja na Shahada za Uzamili na Uzamivu popote pale walipo.
Ameupongeza uongozi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo na Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Tolly Mbwette kwa azma yao njema ya kuanzisha mafunzo ya TEHAMA Zanzibar kwa ajili ya kusaidia jamii kuendana na kasi ya haraka katika maendeleo ya Sayansi na Teknolojia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amefahamisha kwamba huo ni mpango mzuri utakaowasaidia vijana walio wengi pamoja na wananchi wa kawaida wa Zanzibar kwenda na wakati.
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika mpango wake huo kinatarajia kutoa mafunzo ya awali ya matumizi ya kompyuta, Cheti cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) mwaka mmoja na Stashahada ya TEHAMA miaka miwili.
Mapema Mkurugenzi wa Kituo cha uratibu cha Chuo Kikuu Huria Tanzania kilichopo Zanzibar Bw. Yussuf Mhangwa, alisema kituo hicho kina wanafunzi 451, kati ya hao wanafunzik 267 tayari wameshahitimu masomo yao tokea kuanzishwa kwake.
Bw. Yussuf alisema kazi kubwa iliyopo hivi sasa kwa wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho ni kuwawezesha kupata taarifa mbali mbali zitakazowasaidia kuwapa nguvu na uwezo zaidi wa kukabiliana na masomo yao ya kila siku.
Amesema Kituo cha chuo Kikuu Huria cha Tanzania Zanzibar kikiwa miongoni mwa vituo vya mwanzo kuanzishwa na chuo hicho nchini Tanzania, kimekuwa kikitoa mafunzo ya sayansi, sheria, utalii na uchumi katika kiwango cha shahada ya kwanza na ya pili.
Ametoa wito kwa wananchi mbali mbali wa Zanzibar na hasa wale wanafunzi waliomaliza masomo yao ya sekondari, kuitumia fursa hiyo ili kupata taaluma zaidi ya chuo kikuu kwa vile kituo hicho hivi sasa kina uwezo wa kuhudumia wanafunzi 120 kwa wakati mmoja.
Akimkaribisha mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo wa maabara ya mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwenye kituo cha chuo Kikuu Huria Tanzania Beit El Ra,s Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Tolly Mbwette alisema lengo lao ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2014 Mikoa Yote Tanzania iwe na Mfumo huo wa Tehama.
Profesa Tolly aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada zake za kuikubali Taaluma hii ya
Makamu Mkuu huyo wa chuo kikuu huria cha Tanzania alifahamisha kwamba jumla ya wanafunzi 67,103 wamepata taaluma na kufaulu mafunzo yao tokea kuanzishwa kwake mwaka 1993 katika ngazi za stashahada na shahada.