Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam Suleiman Kova akionyesha sare za polisi pea mbili walizokamatwa nazo majambazi saba zikiwa na cheo cha Station Surgeant (Major) ambapo amesema moja ya pea hizo ilikuwa na beji inayosomeka kwa jina la SSGT A.M Mduvike.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam Suleiman Kova akiwaonyesha waandishi wa habari baadhi ya silaha walizokamatwa nazo baadhi ya watuhumiwa wa matukio ya uhalifu kufuatia msako mkali unaoendelea.
Mtuhumiwa anajiyefanya Afisa wa Usalama wa Taifa Alquine Michael Masubo (42) mkazi wa Yombo Buza, ambaye alikamatwa na bastola mbili BROWNING namba A. 956188-CZ83 ikiwa na risasi 12 na MAKNOV namba BA 4799 ikiwa na risasi 19 na kitabu mmiliki wa bastola chenye namba CAR 00071678 chenye jina la P.1827 LT COL Mohammedi H. Ambari.(Picha zote na Geofrey Mwakibete wa Mo Blog).
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeendesha msako mkali na kufanikiwa kukamata watuhumiwa 49 kwa makosa mbalimbali.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova amesema jeshi hilo limemkamata Profesa wa Chuo Kikuu cha DSM Kitengo cha Utafiti wa Mimea Ramadhani Bakari Sensota (63) kwa kosa la kumpuiga risasi na kumjeruhi fundi ujenzi Fadhili Said Mkachino katika maeneo ya Salasala Benako wilaya ya Kinondoni.
Amesema Jeshi hilo pia limekamata majambazi 7 wanaotumia silaha, sare za polisi na redio ya mawasiliano(Radio Call) katika maeneo ya Kiluvya wakiwa na bastola moja aina ya Brown B.3901 ikiwa na risasi 4 na ganda 1 la risasi.
Kamanda Kova ameendelea kusema kuwa pia Jeshi hilo limewakamata watuhumiwa 38 wa madawa ya kulevya aina ya bhangi, ambapo wamekamata Bhangi Kete 37, Bhangi Puli 50, Bhangi Misokoto 67 na Gongo Lita 55.
Ameongeza kuwa pia Jeshi hilo limemkamata mtuhumiwa Alquine Michael Masubo anayejifanya Usalama wa taifa akiwa na bastola 2, moja aina ya Browning ikiwa na risasi 12 na nyumbani kwake alikuta na bastola aina ya MAKNOV ikiwa na risasi 19, kitabu cha mmiliki wa bastola chenye jina la P.1827 LT COL Mohammed H. Ambari, kitambulisho cha JWTZ no. 7001-E. 1075 na Laptop aina ya Toshiba.
Katika muendelezo wa msako huo, Jeshi hilo limewakamata watuhumiwa 2 kwa utapeli waliokuwa wakitumia gari No. T 114 BUJ aina ya NOAH, ambao ni Darusi Mohamedi (35) na Thomas Mashashi.
Pia Jeshi hilo limefanikiwa kumata magari 2 ya wizi namba T 299 BZH –Toyota RV4 na T 831 BZE Toyota RAUM yakiwa yamefichwa katika nyumba anayoishi Aloyce Chuwa (34) fundi simu mkazi wa Ukonga Sabasaba.
Katika hatua nyingine wamekamatwa watuhumiwa 3 Obado Gideon (35), Juma Luka (34) na Marko Yalamula wote wakazi wa Geza Ulole Kigamboni, wakiwa na Pampu moja ya kusukumia maji mali ya Augustino Joseph mkazi wa Vumilia Ukooni Kigamboni.
Aidha Kamishna Kova amesema watuhumiwa 2 wa wizi wamekamatwa wakiwa na Kamba, Plasta na Pingu na kuwataja kuwa ni Sudi Abdallah (32)mkazi wa Yombo na Tausive Mustafa (23) mhindi.
Watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.