Quantcast
Channel: MO BLOG » Admin
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1758

Maoni: Serikali tatu au muungano halisi kipi kinatakiwa?

$
0
0

SAM_4605

Dr.Kilahama -Mwenyekiti, Kamati ya Misitu Duniani chini ya FAO na Mkurugenzi Mstaafu-Idara ya Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Jamhuri wa Muungano Tanzania.

Na Dkt. Felician Kilahama,

Kwanza nianze kwa kuishukuru Tume ya kutayarisha rasimu ya Katiba mpya iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Mheshimiwa Sinde Wariaoba, kwa kazi nzuri waliyofanya.

Nawapongeza Wajumbe wote wa Tume kwa sababu kwa kupitia kwao tumeweza kupata rasimu ya Katiba ambayo kwa kiasi fulani imekoga nyoyo za Watanzania na pia kuzua mjadala mkubwa hasa kwa suala la kuwepo Serikali Tatu.

Ukweli ni kwamba Watanzania walio wengi wamezaliwa baada ya nchi inayoitwa Tanzania kuanzishwa mwaka 1964.

Taifa hili liliwekwa kwenye ramani ya Africa na Dunia kwa ujumla baada ya waanzilishi wake: aliyekuwa Rais wa Tanganyika na aliyekuwa Rais wa Zanzibar kukubaliana kuanzisha nchi inayoitwa Tanzania. 

Wazee wetu hao (sasa wote ni marehemu) walichokifanya ni kuchukua udongo kutoka Tanganyika na udongo kutoka Zanzibar na kuuchanganya hivyo kuashiria kuanzishwa taifa linalojulikana Tanzania. Jina hili limetokana na majina ya iliyokuwa Tanganyika na iliyokuwa Zanzibar. 

Baada ya kutanganza kuanzishwa kwa taifa jipya “TANZANIA” viongozi hao “Rais wa Tanganyika” na Rais wa Zanzibar” hawakuishia hapo tu bali walienda mbele kidogo na kukubaliana jinsi gani taifa hilo jipya litakavyoongozwa au kutawaliwa.

Hivyo wakaingia makubaliano (agreement) ya kuiongoza na kuitawala Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (United Republic of Tanzania) na kuitangaza kuwa dola huru na yenyemamlaka kamili.

Kwa kufanya hivyo mipaka ya awali ya Tanganyika na iliyokuwa ya Zanzibar ikafutwa na kuunganishwa na kuwekwa mipaka mipya ya Tanzania. Vilevile walikubaliana kuwa Rais wa Tanganyika awe Rais wa Tanzania (kiongozi wa nchi) na aliyekuwa Rais wa Zanzibar akawa Makamu wa Rais. Hivyo Taifa la Tanzania likaanzishwa rasimi tarehe 26 Aprili 1964.

Baada ya kuanzishwa Tanzania na kukubaliana jinsi Uongozi wa juu utakuwaje, pia Viongozi hao walikubaliana pamoja kuwa kwa kuunganisha nchi hizo mbili pamoja haitakuwa busara kwa Zanzibar kuingia jumlajumla katika muungano.

Kwa mtazamo huo Zanzibar ikapewa uhuru wa kuendesha mambo yake ya ndani chini ya Rais wa Zanzibar. 

Hivyo pamoja na Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, akaendelea kuiongoza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Wakati huo huo iliyokuwa Serikali ya Tanganyika ikafutwa na kuwekwa chini ya utawala wa Serikali ya Muungano.

Hapa ndipo mushikeli unapoanzia wa kuhoji je, ni kweli huo muungano wa nchi mbili (Tanganyika na Zanzibar) ni muungano halisi au ni kiini macho? Vilevile, yapo mambo muhimu yaliyowekwa bayana kuwa ni masuala ya muungano na kukubaliana kuwa yatashughulikiwa na Serikali ya muungano? Baadhi ya mambo hayo muhimu ni pamoja na masuala ya Ulinzi na Usalama kitaifa na Mambo ya ndani (Polisi, Uhamiaji, Magereza nakadhalika).

Masuala mengine muhimu yalikuwa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; masuala ya Bandari na mengineyo. Hivyo wakati wa kuanzisha muungano masuala yaliyokubaliwa kuwa chini ya mamlaka ya muungano yaliorozeshwa na kufikia kumi na moja ingawa baadaye yalikuja kuongezeka na kufikia ishirini na mawili na pengine hadi sasa ni zaidi ya hayo.

Kwa mantiki hiyo Serikali ya Muungano iliundwa na kuendeshwa kimuungano lakini  ikibeba Wizara nyngine ambazo hazikuwa zinashughulikia masuala ya muungano.

Ukiondoa Wizara zinazoshughulikia masuala yaliyoorozeshwa chini ya muungano bado kuna nyingine kama Elimu, Maji, Kilimo, Mifugo, Maliasili, Afya, Miundombinu, Tawala za mikoa na serikali za mitaa, Utamaduni na Michezo, Kazi na Ajira, Jinsi, Wanawake na Watoto zinatekeleza majukumu yake ndani ya serikali ya Tanzania wakati si za muungano.

Hali halisi ni kwamba Wizara hizo na Mashirika yake zimekuwa zikifanya kazi za Tanganyika lakini bila ya mwelekeo maalumu wa uwajibikaji kitanganyika ila kimuungano?  Wakati inafanyika hivyo kwa Tanganyika, Zanzibar ilibaki na mwelekeo wa kiinchi ingawa ilikuwa ndani ya muungano.

Ni kweli usiopindika kuwa Rais wa Jamhuri wa Muungano anachaghuliwa na wananch wa sehemu zote mbili za muunganio: Tanganyika (maarufu sasa kama Tanzania Bara) na Zanzibar lakini Rais wa Zanzibar anachaguliwa na Wazanzibari ambao wamekwenda mbele zaidi na kuwa na hata vitambulisho maalum vya Uzanzibari lakini wanaishi ndani ya muungano. Siyo hivyo tu bali pia, Zanzibar inayo Katiba yake inayosimamiwa kizanzibar.

Kwa mantiki hiyo hakuna Waziri wa Wizara ya muungano isiyo na majukumu ya kimuungano ambaye anaweza kwenda Zanzibar akawajibika kwa shughuli za wizara anayoiongoza. Sasa cha ajabu nikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano baada ya kuchaghuliwa anapounda serikali ya Muungano sehemu kubwa ya Serikali inasheheni Wizara ambazo hazifanyi kazi kimuungano lakini tunaziita ni Wizara za Serikali ya Muungano.

Ukiliangalia kwa undani zaidi suala hili utagundua kuwa kwa sehemu kubwa inayojulikana ni Serikali ya Muungano wa Jamhuri ya Tanzania inafanya kazi ambazo zingefanywa na Serikali ya Tanganyika.

Kimuundo tunayo Serikali kuu ya Jamhuri wa Muungano (Tanzania) yenye nafsi kuu mbili: Tanzanyika na Zanzibar ila tofauti ni kuwa nafsi moja iko hai (Zanzibar) na nafsi ya pili (Tanzanyika) imekufa au imemezwa ndani ya Muungano. 

Kwa mtazamo huo sasa tusema nini juu ya hayo? Kwamba ilikosewa kuunganisha nchi hizo mbili na kufanya muundago?-HAPANA; kwamba  ilikosewa kuzifuta Tanganyika na Zanzibar kwenye ramani ya dunia na kuiingiza Tanzania lakini wakati huohuo kuiacha Zanzibar ikiwa na Utawala unaotambulika kikatiba wakati siyo nchi rasimi kwa mantiki ya kutoimeza na kuifanya isahaulike kidunia wakati mwenzake amepoteza uhalali wa kuwepo ilikuwa sahihi au siyo sahihi?

Mimi siyo mwanasiasa wala mwanataaluma katika nyanja ya siasa na masuala ya katiba za nchi bali ni mwanamazingira hususani uhifadhi wa misitu na bioanuai, ambavyo ni vitu muhimu sana kwa ustawi wetu na taifa letu kuweza kujiletea maendeleo endelevu. Pamoja na hayo nimevutiwa kulijadili hili kwa nia ya kuweka mawazo yangu bayana kama Mtazania wa kawaida. 

Inawezekana kwa sababu moja au nyingine nikawa na mtazamo tofauti na walio wengi  maana sehemu kubwa ya Watanzania wamezaliwa wakati Tanganyika imeisha kuwa sehemu ya Tanzania (hasa wa Bara) ingawa wa Zanzibari wengi nao wamezaliwa katika kipindi cha muungano lakini wanaufahamu mzuri wa kuiona Zanzibar kama nchi kulingana na mazingira yaliyoanzisha muungano. Kwa mtazamo wangu na kwa uelewa nilionao  naweza kusema kuwa yafuatayo ni bayana juu ya muungano wa nchi za Tanganyika na Zanzibar (kuwepo Jamhuri ya Muungano ya Tanzania) kwamba: 

(i)       Wakati huo (mwaka 1964) ilikuwa muhimu sana kwa Tanganyika na Zanzibar kuungana na hasa kwa sababu za kiusalama na kulinda uhuru wa mataifa hayo mawili.  Sababu hiyo bado ni muhimu sana hata leo maana inabidi tuimarishe ulinzi na usalama wetu hata kama vitisho dhidi ya ubeberu vimepungu lakini kuna vitisho vya kigaidi, madawa ya kulevya, majangiri na kadhalika;

(ii)      Wakati muungano unaanzishwa watanganyika walikuwa wachache lakini pia uelewa wao juu ya muungano haukuwa kama ilivyo sasa. Haikuwa rahisi kuhoji kwa nini tuungane na imani kwa viongozi wao ilikuwa kubwa sana;

(iii)     Mfumo wa utawala wa vyama vingi ulikuwa haupo hivyo Chama kimoja kilitawala na ilikuwa rahisi kupitisha sera na miundo ya kutawala bila kuwepo upingamizi mkubwa. Ndiyo maana waasisi wa muungano waliweza kusonga mbele bila ya kizuizi chochote;

(iv)     Mfumo wa muungano ulikuwa wa masuala muhimu tu na haikuwa jumlajumla kwa mambo yote yaliyokuwa chini ya serikali ya Tanganyika au Zanzibar kuingizwa ndani ya shughuli zaa muungano. Kimsingi haukuwepo muungano wa nchi kama nchi bali ni MAKUBALIANO MUHIMU (agreements) kati ya ma-Rais wa nchi hizo mbili. Makubaliano hayo ya ushirikiano yakawekwa kama msingi wa kuunda muungano uliozaa Tanzania na hatimaye kuimeza Tanganyika lakini kubakiza Zanzibar ikiwa na mfumo wake wa kiutawala. Hali hii ilikwa inakubalika wakati huo lakni kadri tulivyozidi kusonga mbele kumekuwepo na kuzuka kwa maswali ya hapa na pale kuhusu hatima ya Tanganyika ndani ya mfumo wa muungano. 

Watanzania wa leo na katika mfumo wa utawala tulionao hasa kwa kuzingatia siasa za vyama vingi na utandawazi na kwa mantiki ya kuwa wawazi (transparent) na masuala ya haki za binadamu na utawala wa sharia, wanataka kujua huu muungano tulio nao maanake nini?

Kwa mtazamo wangu sula siyo serikali tatu au mbili bali ni kuwepo mfumo wa muungano utakaotoa haki sawa kwa pande zote mbili za muungano kuweza kunufaika na kuwepo na muungano na siyo kuubeba upande mmoja na kuukandamiza upande mwingine. 

Kama kweli nchi hizo mbili (Tanganyika na Zanzibar) ziliuungana kikwelikweli na kuwepo dhamira sawa kwa nini kusiwepo na serikali moja ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania?  Tunapoendelea na mawazo kuwa Zanzibar iendelee kuwa na utawala wake ndani ya mfumo wa muungano ni sawasawa na kusema kuwa hakuna muungano halisi bali yapo Makubaliano Maalum ya kushirikiana kati ya Tanganyika na Zanzibar. 

Ni vema suala hili tukalitazama kwa undani Zaidi na kwa pamoja tukakubaliana na mfumo maalum wa kushughulikia na kutekeleza masuala ya muungano. 

Kinyume cha hapo hatutakuwa wakweli bali ni kupindisha mambo tu na kusema kuna serikali ya muungano wakati ni serikali ya Tanganyika ikiwa imevaa sura ya muungano wakati hali halisi siyo hivyo.  Nazidi kujiuliza kuwepo taifa la Tanzania katika upana na urefu wa suala zima la muungano je, changamoto kubwa ni kuwepo serikali tatu, serikali mbili, muungano halisi au ni nini hasa?

Mwisho niwaombe watanzania wenzangu kuwa suala la muungano tusilibeze ni siuala muhimu sana na nyeti ila tulijadili kwa kina kwaa mantiki ya kuweza kupata mfumo wa utawala utakaoimarisha muungano wetu. 

Kwa kupitia mchakato wa kuipata Katiba nyingine niwaombe Waheshimiwa Wabunge wa BUNGE MAALUM LA KATIBA walijadili suala hili kwa umakini mkubwa na ikiwezeka vipingamizi vinavyozuia kuwepo na muungano halisi kwa kupitia Katiba inayojadiliwa viweze kuondolewa na hivyo kuiwezesha Tanzania kuwa nchi pekee dunia yenye muungano wa kweli na si vinginevyo.  Waheshimiwa Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wasijadili suala la muungano kwa msukumo wa vyama au makundi yao kwa nia ya kukidhi haja za vyama vyao au makundi bali iwe ni kwa faida ya kuwepo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yenye manufaa kwa watu wake wote: Tanzania kwanza na mengine baadaye.

Waheshimiwa Wabunge watende haki na kuwa wakweli na wazungumze kwa hekima na busara kubwa bila ya kuwa na jaziba wala mtimanyongo wakati wa kujadiliana suala la muungano nna hatimaye tupate Katiba itakayokidhi matakwa ya watanzania wengi.  MWENYEZI MUNGU IBARIKI TANZANIA, DUMISHA UHURU NA MSHIKAMANO KWA WATU WAKE WOTE.  Hakuna lisilo wezekana kama kweli tunaamini kuwepo na Muungano halisi kati ya Tanganyika na Zanzibar basi taifa lililozaliwa kwa kuziunganisha nchi hizo mbili liwe ni taifa kamili na kwelikweli-TANZANIA. Yote yawezekana kwake anayeamini hivyo.  KILA LILILOJEMA KWA WAJUMBE WOTE  WA BUNGE MAALUMU LA KATIBA.

Dr Kilahama -Mwenyekiti, Kamati ya Misitu Duniani chini ya FAO na Mkurugenzi Mstaafu-Idara ya Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Jamhuri wa Muungano Tanzania.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 1758

Trending Articles