Mradi wa Masuala ya Kijinsia kutoka Shirika la Plan International, Bi.Anna Mushi Mshauri akitoa maelezo kwa wandishi wa habari juu ya mafanikio ya mradi wa mMama na mwana wilayani Sengerema. Kulia ni mwandishi wa Redio Sengerema Dullah Julius.(picha na Daniel Makaka Sengerema).
Bi Anna Mushi akimwelekeza jambo msimamizi na mfuatiliaji wa mradi ya Shirika la Plan International Bi Joelle Siemens walipotembelea kijiji cha Kasisa wilayani Sengerema.
Mratibu wa Shirika la Plan International wilayani Sengerema Bw. Gaspar Tisiani (kulia) akisaidiana na wahudumu wa Afya kupima uzito watoto.
Na Daniel Makaka, Sengerema
WAKINAMAMA wajawazito nchini wameombwa kujijengea tabia ya kuhudhuria Kliniki kwa muda wote wa ujauzito ili kuepusha vifo vinavyoweza kuepukika wakati wa kujifungua.
Akiongea na akinamama waliohudhuria kliniki katika Zahanati za Kasisa na Nyakasungwa zilizopo Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza, kwa ajili ya zoezi la utoaji wa chanjo ya kuzuia kuhara na kutapika, upimaji wa uzito na semina ya lishe ya mama na mtoto kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 5, lililofanyika Novemba 21 mwaka huu.
Bi.Anna Mushi ambaye ni mshauri wa Mradi wa Masuala ya Kijinsia kutoka Shirika la Plan International, amesema mama mjamzito anapaswa kuhudhuria kliniki na kuhakikisha kuwa anafuata taratibu wanazopewa kutoka kwa watalaamu.
Ameongeza kuwa, pindi mama anapojifungua kuhakikisha kuwa mtoto anapata maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita (6), ili kuweza kujenga Afya ya Ubongo wa mtoto kwa kuzingatia ratiba ya chakula anachokula mama wakati wa kunyonyesha.
Aidha Bi.Mushi amewataka akina baba kuwa mstari wa mbele kwa kuwapeleka akinamama kliniki na kuhakikisha kuwa wanawapa muda wa kupumzika kipindi cha ujauzito na wakati wa kunyonyesha.
Sanjari na hayo naye, Mratibu wa Mradi huo wa Plan International wilayani Sengerema, Ndg. Gasper Tisian amewaasa wakinababa wanaohudhuria kliniki kwa kuwapeleka wakinamama na watoto kuwa mabalozi kwa wengine juu ya kujali afya ya mama na mtoto.