Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe akiwa amesimama juu ya mradi wa maji wa Miganga, pembeni yake akiwa na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde katika ziara aliyoifanya Wilayani Chamwino, mkoani Dodoma.
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe akiwa pembeni ya mradi wa maji wa Mvumi Misheni, pembeni yake akiwa na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde katika ziara aliyoifanya Wilayani Chamwino, mkoani Dodoma.
Tanki la maji la mradi wa maji wa Mvumi Makulu, katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma likiwa katika hatua za mwisho kukamilika, katika ziara iliyofanywa na Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe wilayani hapo.
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe (katikati) akiwa amesimama mbele ya tanki la maji la mradi wa Mvumi Makulu, pamoja na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino (kushoto), Fatuma Ally katika ziara iliyofanywa na Waziri huyo wilayani hapo.
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Mhandisi wa mradi wa maji wa Mvumi Makulu, Wilayani Chamwino (kulia), katika ziara aliyofanya Waziri huyo wilayani hapo.
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mvumi Makulu katika ziara ya kukagua miradi ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.
Mkurugenzi wa Idara ya Maji Vijijini, Wizara ya Maji, Mama Frida Rweyemamu akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mvumi Makulu, katika ziara ya Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe wilayani Chamwino.
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe ameendelea kuchukua hatua kuhakikisha Matokeo Makubwa ‘Big Results Now’ kwa sekta ya maji yanafikiwa kwa kufanya ziara ya kukagua miradi ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, mjini Dodoma mwishoni mwa wiki hii.
Waziri Maghembe ambaye alifanya ziara hiyo, katika moja ya mikakati kuhakikisha miradi yote ya maji inatekelezwa kwa haraka na ufanisi mkubwa. Alifanya ziara hiyo baada ya kuombwa na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde kwenda kuangalia maendeleo ya miradi ya maji katika Halmashauri ya Wilaya hiyo mpya.
“Haraka haraka ndio Baraka, hatuna budi kuachana na utamaduni wetu wa zamani kuhakikisha Big Results Now inafikia malengo yake kwa kasi na ufanisi mkubwa. Milioni 200 zimetengwa kwa ajili ya kutatua tatizo la maji Chamwino, na tutaleta wahandisi kuja kuangalia tatizo ni nini na kulipatia ufumbuzi mara moja”, alisema Prof. Maghembe.
“Nawapongeza Shirika la Maji na Maendeleo Dodoma (MAMADO) kwa kushirikiana na Serikali na nasisitiza maendeleo yataletwa na wananchi wenyewe na sio kutegemea misaada siku zote”, aliongeza Prof. Maghembe.
Waziri Maghembe alifurahishwa sana na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo na kuahidi kuhakikisha changamoto zinazojitokeza katika kuekeleza miradi zinatatuliwa, ikiwemo kutoa fedha kwa ajili ya kutatua tatizo la ukosefu wa fedha kwa miradi hiyo inayoendelea ya halmashauri hiyo, ili iweze kukamilika kwa wakati.
Mbunge wa Jimbo hilo, Livingstone Lusinde alimshukuru sana Prof. Maghembe kwa kuitikia wito wake kuja kutembelea wilaya hiyo na kuja kujionea mwenyewe hali halisi ya maji kwa wakazi wa eneo hilo na kuwasisitizia wananchi kuwa Serikali inafanya juhudi kubwa kutatua kero hiyo na kukaa tayari kupokea huduma hiyo kwa kiwango cha kuridhisha.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Fatma Ally, alisema yeye atashirikiana bega kwa bega na Serikali na kusimamia kwa ukaribu miradi hiyo na kuhakikisha inatekelezwa kama ilivyoagizwa na kuleta faraja kwa wakazi wa Chamwino ambalo wana heshima ya kuwa na Ikulu ndogo ya Rais.
Ziara hiyo ilijumuisha miradi ya vijiji vya Miganga, Mvumi Misheni na Mvumi Makulu. Kati ya vijiji hivyo, vijiji vya Mvumi Misheni na Mvumi Makulu ni kati ya vijiji kumi ambavyo viko katika mpango kupatiwa maji kupitia program ya Big Results Now.
Moja ya hatua zilizochukuliwa ni kuchimba visima virefu na usambazaji wa maji na ujenzi wa miundombinu ya maji, na mpaka sasa ujenzi wa miundombinu ya maji unaendelea katika kijiji cha Mvumi Makulu na uchimbaji wa kisima kirefu na usanifu wa miundombinu wa maji umekamilika, ukibaki mchakato unaoendelea kumpata mkandarasi wa ujenzi katika kijiji cha Mvumi Misheni.
Miradi ya Miganga na Mvumi Makulu pekee inategemea kuhudumia watu 14,730 baada ya kukamilika.
Katika ziara hiyo Waziri wa Maji aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Fatuma Ally, Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde na Mkurugenzi wa Idara ya Maji Vijijini, Wizara ya Maji, Bi. Frida Rweyemamu na baadhi ya maafisa wa Wizara hiyo na kuona hatua iliyofikiwa katika mkakati wa kuhakikisha kero ya maji inafikia kikomo wilayani Chamwino na vitongoji vyake.