Majeshi ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamedhibiti maeneo ya vilima vilivyopo karibu na mji wa Goma Mashariki mwa nchi hiyo, baada ya wapiganaji wa kundi la waasi wa M23 kuondoka eneo hilo.
Waasi wa kundi la M23 wamesema wameondoka eneo hilo la milimani ili kuruhusu uchunguzi huru juu ya mashambulizi ya makombora yaliyosababisha vifo vya raia mjini Goma na katika nchi jirani ya Rwanda.
Rwanda imeishutumu Kongo kwa kufanya mashambulizi hayo kwa makusudi na kuibua wasiwasi kuwa huenda kukawa na makabiliano kati ya nchi hizo mbili.
Wanadiplomasia wa kanda ya maziwa makuu wamesema majeshi ya Rwanda yameonekana yakisafiri kutoka mji mkuu kuelekea kaskazini mwa nchi hiyo.