Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete.
Hussein Makame na Jennifer Chamila, MAELEZO.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete anatarajia kuzindua ujenzi wa barabara na kufungua rasmi kivuko cha Ruvuvu mkoani Kagera.
Taarifa iliyotolewa na Katibu mkuu wa wizara ya Ujenzi Balozi Herbert Mrango kwa yvombo vya habari inasema kuwa Mh. raisi Kikwete atazindua kivuko hicho Julai 27 mwaka huu.
Kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba tani 35 ikiwemo magari madogo 4 na abiria 80 kwa pamoja, kinatoa huduma ya kuvusha magari na abiria katika mto Ruvuvu eneo la Rusumo
Amesema kabla ya ufunguzi wa kivuko hicho, Rais Kikwete ataweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kigoma-Biharamulo-Lusahunga yenye urefu wa kilometa 154, Julai 26 mwaka huu.
Ameongeza kuwa Jumapili tarehe 28 Julai Rais Kikwete ataweka jiwe la msingi katika barabara ya Kyaka-Bugene-Kasumulo yenye urefu wa kilometa 59.1 tukio litakalofanyika katika kijiji cha Omugakorongo.
Amefafanua kuwa miradi yote mitatu inagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba kutekelezwa kwa miradi hiyo itasaidia sekta ya usafirishaji na kukuza uchumi wa mkoa wa Kagera.
Pia barabara na kivuko hicho vitaimarisha huduma ya usafirishaji katika mkoa huo na kuboresha biashara na usafiri kati ya mkoa huo na mikoa mingine pamoja na nchi za Burundi, Rwanda na Uganda