Rais wa zamani wa Afrika kusini Thabo Mbeki amesema mtangulizi wake Mzee Nelson Mandela, huenda akatoka hospitali na kuendelea na matibabu nyumbani.
Mbeki amesema hayo wakati akizungumza katika hafla moja ya Chama cha Afriacan National Congress-ANC.
Mandela amelazwa hospitali kwa wiki tano sasa kutokana na maambukizi ya mapafu, hali iliosababisha kumiminika kwa risala za kumuombea nafuu kutoka ndani ya Afrika Kusini na kimataifa.
Marafiki waliomtembelea wamesema Mandela bado anapumua kwa msaada wa mashine.
Shujaa huyo wa vita dhidi ya sera ya ubaguzi wa rangi, alitumikia kifungo cha miaka 27 gerezani, kabla ya kuwa Rais wa kwanza wa Afrika kusini ya Kidemokrasia mwaka 1994.
Thabo Mbeki aliyekuwa makamu wake wa Rais, alishika wadhifa huo wa kuiongoza Afrika kusini wakati Mandela alipostaafu mwaka 1999.
Ifikapo siku ya Alhamisi wiki hii Mandela atatimia umri wa miaka 95.