Meneja uhusiano wa Airtel Tanzania Jackson Mbando akiongea na waandishi wa Habari wakati wa kutangaza Kliniki ya Kimataifa ya mpira wa soka ya Manchester United ambayo itafanyika Jijini Dar es Salaam April 23-27 chini ya wakufunzi kutoka Klabu ya Manchester United. Kushoto ni Rais wa shirikisho la mpira wamiguu nchini (TFF) Jamal Malinzi. Iliofamyika jijini Dar-es-Salaam.
Rais wa shirikisho la mpira wamiguu nchini (TFF) Jamal Malinzi akiongeana na waandishi wa habari wakati wa kutangaza Kliniki ya Kimataifa ya mpira wa soka ya Manchester United ambayo itafanyika Jijini Dar es Salaam April 23-27 chini ya wakufunzi kutoka Klabu ya Manchester United. Kulia ni meneja uhusino wa Airtel Tanzania Jackson Mbando.
-Ni kutoka nchi 12 Afrika
-Waziri Bernard Membe mgeni rasmi siku ya ufunguzi
-Kliniki kuendeshwa na makocha kutoka Manchester United
Wachezaji wa soka chini ya umri wa miaka 17 kutoka nchi 12 barani Afrika wanatarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam Jumatatu Aprili 21 kushiriki kliniki ya soka ya kimataifa. Hii ni mara ya pili Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa kliniki ya kimataifa baada ya ile iliyofanyika kwenye uwanja wa wa kisasa wa Taifa mwaka 2011.
Kliniki ya mwaka huu itakayofanyika kwenye uwanja wa Azam, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam inakutanisha wachezaji chipukizi, wasichana na wavulana, kutoka nchi za Kenya, Uganda, Malawi, Sierra Leone, Burkina Faso, Chad, Congo Brazzaville, DRC, Niger, Madagascar, Gabon, Seychelles na mwenyeji – Tanzania.
Mafunzo hayo ya siku tano mfululizo chini ya makocha wazoefu kutoka klabu maarufu duniani ya Manchester United yana lengo la kuwapa vijana mbinu mbalimbali za kisoka hasa katika eneo la ushambuliaji.
Kliniki hii ya kimataifa inashirikisha vijana waliofanya vizuri mwaka jana katika mashindano ya Airtel Rising Stars kwenye nchi zao pamoja na washindi wa mashindano ya kimataifa yaliyofanyika nchini Nigeria ambapo timu ya wasichana ya Tanzania ilitwaa uchampioni wa fainali hizo hizo.
Hafla ya uzinduzi wa kliniki hiyo imepangwa kufanyika siku ya Jumatano kwenye uwanja wa Azam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Bernard Membe atakuwa mgeni rasmi. Membe anatarajiwa kuwahamasisha vijana kujituma ili kuweza kuendeleza ipasavyo vipaji vyao vya soka.
Hafla hiyo ya uzinduzi pia inatarajiwa kuhudhuriwa na mabalozi kutoka nchi zinazoshiriki kwenye kliniki hiyo itakayojumuisha mafunzo ya uwanjani na ya darasani. Vipindi vyote hivyo vitafanyika pale pale Azam Complex.
Program ya Airtel Rising Stars ni mpango wa maendeleo ya soka kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 barani Afrika ukidhaminiwa na kampuni ya simu za kiganjaji ya Airtel na kuungwa mkono na Manchester United. Lengo lake ni kusaidia kuibua vipaji vya soka kutoka ngazi ya chini (grassroots) hadi Taifa.