Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa Chama cha Wananchi CUF Salum Bimani akizungumza na waandishi wa Habari kwenye Ofisi yao, Vuga Mjini Zanzibar.
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali wakimsikiliza Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa CUF (hayupo pichani) Salum Bimani katika Ofisi ya Vuga, Mjini Zanzibar.
Mwandishi wa Habari wa ZBC Dennis Bilal akiuliza swali kwenye mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Chama cha CUF Ofisni kwao Vuga, Mjini Zanzibar leo.(Picha na Makame Mshenga wa Maelezo Zanzibar).
Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar
Chama cha Wananchi (CUF) kimeilalamikia Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kutokana na jinsi ilivyosimamia uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki uliofanyika tarehe 2 mwezi huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi ya CUF, Vuga Mjini Zanzibar leo, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa Chama hicho Salim Bimani amesema Uchaguzi huo haukuwa huru na haukuwa wa haki.
Amesema vitendo vya kuvurugwa uchaguzi huo vilianza kujitokeza kuanzia wakati wa kampeni na siku ya uchaguzi lakini pamoja na kutoa taarifa kwa Tume ya Uchaguzi hakuna hatua yoyote iliyochukua.
‘’Chama cha CUF kilibaini tokea mapema maandalizi ya fujo na matumizi mabaya ya nguvu za dola pamoja na Vikosi vya Serikali, ambavyo viliandaliwa kwa dhamira ya makusudi ya kuwapa haki wasiostahiki na pia kuwanyima watu wengi haki yao ya kufanya maamuzi ya kidemokrasi’’, alisema Salim Bimani.
Aliongeza kuwa upo ushahidi kwamba Vikosi vilitumika kuwalinda na kuwasafirisha wapigakura mamluki kutoka sehemu nyengine kuja kupiga kura bila ya hatua yopyote ya kisheria kuchukuliwa.
Bimani alidai kuwa vikosi hivyo vilithubutu kuwatisha baadhi ya wananchi waliopaza sauti kupinga mwenendo huo haramu wa uchaguzi.
“ Wananchi na Chama cha Wananchi, CUF , walijenga matumaini makubwa ya kuona Uchaguzi huru na wa haki ukifanyika katika zama hizi ambazo Zanzibar inaongozwa na Mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, chini ya misingi ya maradhiano ya kisiasa, inayozingatia amani, utulivu, demokrasi na mshikamano kupitia siasa za kistaarabu’’, aliongeza Mkurugenzi Bimani .
Alisema kutokana na kasoro nyingi katika uchaguzi huo mdogo, CUF imekosa imani na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na Daftari la Kudumu la wapigakura kutokana na kuchezewa na halipo kwa misingi ya kutekeleza demokrasia, Haki na Uadilifu.
Bimani alirejea kauli ya Chama hicho kutaka Tume ya Uchaguzi (ZEC) ivunjwe ili kutoa fursa ya kupatikana Mamlaka nyengine huru itakayoweza kusimamia Uchaguzi wa Haki na wa Kidemokrasia.
Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki ulifanyika kufuati kujiuzulu aliekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo Mansour Yussuf Himid mwishoni mwa mwaka jana.