Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili Davos,Uswisi, jioni ya Jumatano, Januari 22, 2014, kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa Mwaka 2014 wa Taasisi ya Uchumi Duniani ya World Economic Forum (WEF).
Kwenye Hoteli ya Sheraton ambako amefikia, Rais Kikwete amepokelewa na mawaziri ambao wataambatana naye kwenye Mkutano huo. Mawaziri hao ni Profesa Jumanne Maghembe ambaye ni Waziri wa Maji; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mheshimiwa Christopher Chiza na Mheshimiwa Harrison G. Mwakyembe, Waziri wa Uchukuzi.
Mkutano huo wa siku nne umeanza leo na miongoni mwa shughuli za Rais Kikwete leo ni pamoja na kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Nigeria, Mheshimiwa Goodluck Jonathan ambaye nchi yake itaandaa Mkutano wa WEF – Afrika utakaofanyika Mei mwaka huu. Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika, mbali ya Afrika Kusini, kuandaa WEF-Afrika mwaka 2010.
Rais Kikwete leo pia atahudhuria kikao maalum kuhusu maji na usalama wake duniani – Water Security Pathfinders: Accelerating Change to Secure Tomorrow’s Water Future kabla ya kukutana na Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza Mheshimiwa Nick Clegg. Baadaye, Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Jetro ya Japan, Bwana Hiroyuki Ishige.
Mchana wa leo, Rais Kikwete atashiriki katika kikao kitakachozungumzia jinsi gani ya kuvunja vikwazo vya maendeleo
Baadaye mchana wa kesho, Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Bwana Bill Gates wa Taasisi ya Bill & Melinda Gates na binadamu anayeongoza kwa utajiri duniani kabla ya kukutana na Bwana Gates, Rais Kikwete atakutana kwa mazungumzo na Profesa Klaus Schwab, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa WEF.