Quantcast
Channel: MO BLOG » Admin
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1758

Polisi Arusha yazidi kuimarisha vikundi vya Ulinzi Shirikishi

$
0
0

GEDSC DIGITAL CAMERA

Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii mkoa wa Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Mary Lugola akimkabidhi kizibao mmoja wa walinzi wa kikundi cha Ulinzi Shirikishi cha Muklati kilichopo Ngaramtoni wilayani Arumeru. (Picha na Rashid Nchimbiwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha).

GEDSC DIGITAL CAMERA

Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi (SSP) Mary Lugola akiwa pamoja na viongozi wa Ngaramtoni wakionyesha moja ya kizibao kilichoandikwa “ULINZI SHIRIKISHI MKOA WA ARUSHA” Pichani kushoto ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Elibariki Kileo ambaye ni Polisi Tarafa katika eneo hilo. Jumla ya vizibao 15 vimekabidhiwa kwa kikundi cha Ulinzi shirikishi cha tarafa ya Muklati.(Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha).

GEDSC DIGITAL CAMERA

Askari wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi na askari wa kikundi cha Ulinzi Shirikishi cha Muklati kilichopo wilayani Arumeru. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha).

Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Katika kile kinachooneka kuzidi kuhamasisha na kuimarisha Ulinzi na Usalama maeneo mbalimbali ya Mkoa huu, Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Polisi Jamii mkoani hapa limetoa vizibao 15 kwa kikundi cha Ulinzi Shirikishi cha Muklati kilichopo Ngaramtoni wilayani Arumeru.

Akizungumza wakati wa makabidhiano wa vizibao hivyo leo tarehe 08.01.2014 Adhuhuri, Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Mary Lugola alisema kwamba, Jeshi hilo limeonyesha njia ili kuweza kuwahamasisha wananchi wa maeneo mbalimbali mkoani hapa waweze kuunga mkono juhudi hizo hivyo kujitolea kwa ajili ya kusaidia vikundi hivyo.

Alisema kikundi hicho kilichopo Ngaramtoni kimeweza kuhakikisha eneo hilo linakuwa salama na hali hiyo inatokana na uzalendo walionao vijana hao. Alisema elimu ya ulinzi waliyopata vijana hao imewawezesha kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu hali ambayo imesaidia kupunguza vitendo vya uhalifu na kufanikiwa kukamata silaha mbalimbali zilizotengenezwa kienyeji.

Mkuu huyo wa Polisi Jamii aliendelea kusema kwamba, vizibao hivyo vyenye maandishi ya “ULINZI SHIRIKISHI MKOA WA ARUSHA” vitawasaidia kwenye utendaji wao wa kazi hasa katika suala la utambulisho. Alisema ni vigumu kumtambua mtu au kutambuana mara moja lakini kupitia vizibao hivyo wananchi wa eneo hilo watawatambua kiurahisi na wao kutambuana.

Naye Polisi Tarafa wa eneo hilo ambaye pia Mkuu wa kituo cha Polisi Ngaramtoni, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Elibariki Kileo alizidi kuwasisitiza wananchi wa Tarafa hiyo wajitokeze katika kusaidia kikundi hicho na vingine vilivyopo katika mitaa na vitongoji mbalimbali vya Tarafa hiyo kwani usalama uliopo katika eneo hilo ni matunda ya kikundi hicho.

Aidha kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Muklati Bw. Naima Saitabao alisema kwamba toka kikundi hicho kianzishwe mwaka 2007 hali ya uhalifu imezidi kupungua ikilinganishwa na kipindi cha nyuma. Alisema ushirikiano uliopo kati ya Polisi Tarafa wa eneo hilo, uongozi wake pamoja na wananchi uliwezesha kuanzisha kikundi hicho ambapo kimeweza kudhibiti matukio mengi ya uhalifu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.

 


Viewing all articles
Browse latest Browse all 1758

Trending Articles