![DSC02914]()
Mjumbe wa halmashauri kuu (NEC) CCM taifa manispaa ya Singida, Hassan Mazala akizungumza muda mfupi kabla ya kukabidhi zawadi kwa washindi watatu wa ligi ya kuwania zawadi ya shilingi Laki Moja.
![DSC02894]()
Mjumbe wa halmashauri kuu (NEC) taifa manispaa ya Singida, Hassan Mazala akikagua timu ya kitongoji cha Ngaida kabla timu hiyo haijaumana na Kisaki ‘A’ kwenye mechi ya fainali ya kuwania zawadi ya shilingi Laki Moja.
![DSC02906]()
Baadhi ya viongozi wa ngazi ya CCM manispaa ya Singida wakifuatilia kwa makini mchezo wa fainali kati ya timu ya Kisaki ‘A’ na Nag’aida uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Kisaki.
![DSC02903]()
Baadhi ya wapenzi wa soka wa kijiji cha Kisaki manispaa ya Singida wakishuhudia mchezo wa fainali ya kuwania zawadi ya shilingi Laki Moja zilizotolewa na uongozi wa CCM kijiji cha Kisaki.
![DSC02901]()
Timu ya Kisaki ‘A’ iliyojinyakulia zawadi ya shilingi Laki Moja baada ya kuifunga Ng’aida magoli 3-1 kwenye fainali iliyofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Kisaki.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu
MJUMBE wa halmashauri kuu CCM (NEC) manispaa ya Singida, Hassan Mazala amewataka vijana wanaoshiriki michezo mbalimbali kuanzisha vikundi ili kujijengea mazingira mazuri ya kukopesheka na taasisi za kifedha.
Mazala ametoa changamoto hiyo wakati akizungumza muda mfupi kabla hajakabidhi zawadi kwa washindi wa ligi ya soka ya kijiji cha Kisaki manispaa ya Singida. Ligi hiyo ilishirikisha timu sita za vitongoji vya kijiji cha Kisaki.
Alisema vijana na hata watu wengine ili kupata mikopo au misaada ya kupambana na adui umaskini kwa njia rahisi isiyokuwa na masharti magumu,ni kujiunga kwenye vikundi.
Katika hatua nyingie, Mazala aliupongeza uongozi wa CCM kijiji cha Kisaki kubuni na kuanzisha ligi ya soka kwa lengo la kuwaunganisha vijana na kuibua vipaji vyao.
“Kama risala yenu ilivyosema kuwa lengo la ligi hii, ni kuwanusuru vijana na vitendo vya Ulevi wa kupindukia, Uzururaji, Ngono zembe, ujambazi na matumizi ya madawa ya Kulevya. Uamuzi wenu ni wa busara sana, vijiji vingine vinapaswa kuiga mfano wenu,” alisema Mazala.
Timu zilizoshiriki ligi hiyo iliyoanza agosti 18 mwaka huu,ni Kisaki A, Kisaki B, Kitope, Irao, Iyangi na Ng’aida.
Timu za Kisaki A na Ng’aida ndizo zilizofanikiwa kucheza fainali ya ligi hiyo na Kisaki A ilishinda mechi hiyo kwa kuifunga Ng’aida magoli 3-1.
Kwa ushindi huo, Kisaki A ilijinyakulia shilingi laki moja na mipira mitatu, mshindi wa pili Ng’aida, ilipata shilingi 70,000 na mshindi wa tatu Kitope iliambulia shilingi 30,000.
Mazala, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika fainali hiyo ametoa msaada wa mipira saba na shilingi 50,000 kwa timu zilizoshiriki.