Kiongozi wa kihistoria wa kundi la upinzani nchini Burundi Agathon Rwasa , anakusudia kujitokeza hadharani kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka mitatu na kutangaza mipango yake ya kugombea kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Kiongozi wa kundi la zamani la waasi la National Liberation Forces (FNL) alikimbia kutoka Burundi na kwenda kuishi mafichoni baada ya yeye pamoja na upinzani nchini humo kupinga uchaguzi wa mwaka 2010 kuwa ulikuwa wa udanganyifu.
Serikali ya nchi hiyo ilimuona kuwa kitisho tangu wakati huo, lakini Rwasa amerejea mjini Bujumbura siku chache zilizopita baada ya kupata uhakikisho kuhusu usalama wake.
Msemaji wake Aime Magera amesema kuwa Rwasa mwenye umri wa miaka 49 anatarajiwa kujitokeza hadharani mbele ya wafuasia wake pamoja na maafisa wengine mashuhuri, ikiwa ni pamoja na wanadiplomasia wa mataifa ya kigeni.
Hakufahamika yuko wapi tangu wakati huo, ambapo mara kadhaa aliripotiwa kuonekana katika nchi za jirani katika eneo la Kivu ya kusini katika jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, pamoja na Tanzania na Zambia.