Mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika mkoa wa Pwani, imesababisha madhara mengi, ikiwemo kuharibu vibaya kipande cha barabara kinachoanzia bwalo la magereza hadi nyumba za Tamco katika halmashauri ya manispaa ya Kibaha. Kipande hicho endapo hakitafanyiwa matengezo mapema,kuna kila dalili kwamba kitakuwa hakipitika kabisa na hivyo kukata mawasiliano kati ya wakazi wa nyumba za Tamco, maeneo ya makaburi ya Air Msae na vitongoji vingine na makao makuu ya manispaa hiyo.(Picha na Nathaniel Limu aliyekuwa Kibaha).
Na Nathaniel Limu (aliyekuwa Kibaha)
BAADHI ya wakazi wa nyumba za TAMCO na maeneo ya makaburi ya Air Msae, wameiomba halmashauri ya manispaa ya Kibaha, kukifanyia matengenezo mapema kipande cha barabara kinachoanzia bwalo la magereza hadi nyumba za Tamco, ili kunusuru usalama wao pamoja na mali zao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hii, wamedai kipande hicho kimeharibika vibaya kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hivi sasa mkoani Pwani.
Wakifafanua,wamesema kwamba kutokana ba barabara hiyo kutokuwa na mifereji ya kumwaga maji ya mvua nje ya barabara,kwa sasa kumezuka mito ya kupitisha maji ya mvua inayoendelea kunyesha.
Wamedai kwamba maji ya mvua kwa sasa yanaendelea kuimomonyoa barabara na kusababisha ipitike kwa taabu kubwa.
“Kwa magari madogo ndio imekuwa tatizo kubwa, baadhi ya sehemu ya kipande hicho cha barabara,inabidi upite kwa tahadhari kubwa kwa sababu sehemu ya chini ya gari,hukwangua ardhi”alisema mmoja wa wakazi wa nyumba za Tamco Mohammed Kinanda.
Akifafanua zaidi,alisema kipande hicho kisipofanyiwa matengenezo,kinaweza kuharibika zaidi na kusabisha kisipitike kabisa.
Kinanda alisema kipande hicho endapo kitafikia hatua ya kutokupitika,kitasababisha mawasiliano kati ya wakazi wa nyumba za Tamco,maeneo ya makaburi ya air Msae na vitongoji vingine na makao makuu ya manispa ya Kibaha,yatakatika.
“Kipande hicho ambacho sehemu kubwa imeharibika vibaya,kinapaswa kifanyiwe ukarabati mapema iwezekanavyo.Barabara hii ikijifunga/kufungwa,itasababisha madhara mengi ikiwemo wagonjwa na akina mama wajawazito itakuwa vigumu kuwawahisha katika vituo vya kutolea huduma ya afya”,alisema mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Juma.